UJASIRI ni hadithi kuhusu changamoto anazopitia mtoto wa kiume. Ni hadithi ambayo imemchora mtoto wa kiume kama mtu jasiri ambaye anaweza kufaulu licha ya kukumbwa na changamoto nyingi katika maisha.
Inamhimiza mtoto wa kiume kutokata tamaa, kuwa na matumaini na pia kuwa na ruwaza ya kufanikiwa maishani. Mwanamume / mtoto wa kiume anahitaji kutiwa moyo, kushikwa mkono katika safari ya maisha na ataweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii, kama vile tunavyomwona mhusika mkuu Bwana Suluhu akikumbwa na masaibu mengi kama vile: kuchomewa nyumba, kufukuzwa nyumbani, uchochole uliokithiri ,bibi yake kutoroka na kumwachia jukumu la kuwalea wanao peke yake, kuugua saratani na kuweza kuishinda na kupona, kuachwa na bibi wa pili na masaibu mengine mengi lakini licha ya haya yote alijikaza kisabuni na akaweza kufanikiwa mwishoni. Kupitia hadithi hii tunaona kwamba kila kitu kinawezekana sio tu kwa wanaume bali kwa yeyote aliye na ujasiri na msukumo wa kufaulu maishani. Tunahimizwa tusife moyo kwani tukijitahidi tutaweza kushinda changamoto zote.