Jamii ya leo inakumbwa na uozo wa maadili. Tamaa, ubinafsi na unafiki umetawala mioyo ya wengi. Ndani ya giza hili la kimaadili, usaliti huzaliwa na kustawi ukiangamiza haki na kuvunja misingi ya uaminifu. Baada ya kifo cha ghafla cha Bw. Mambo jijini Nairobi, binti yake Fauna anakataa kukubali kimyakimya kilichofunika tukio hilo. Akiwa na huzuni moyoni lakini pia azma thabiti, anafunga safari kutoka kwao Mombasa hadi Nairobi kutafuta ukweli uliositirika gizani. Kadri anavyochimba, anagundua kwamba nyuma ya kifo cha babake, kulikuwa na mtandao wa siri na njama zilizofichwa chini ya kivuli cha usaliti. Hata hivyo, anakumbana na changamato na vikwazo ambavyo vinalemaza azma yake. Je, atafanikiwa kufichua ukweli na kupata haki au naye pia atamezwa mzimamzima na jinamizi lililommeza babake ghafla?
‘…majibu yalihitajika, majibu hayo ndiyo yangeleta mwanga wa ukweli uliokuwa umefichwa kwenye giza la uhalifu.’
Ni mwandishi na mwalimu mwenye shahada ya ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Moi. Amefundisha katika shule mbalimbali; Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu, Shule ya Upili ya Baringo, Shule ya Upili ya Nakuru na Shule ya Upili ya Wasichana ya Icuga katika kaunti ya Nyeri anakofundisha hivi sasa. Ari yake katika fasihi imejitokeza katika kazi zake ambapo ameandika mashairi, riwaya Donda la Maisha, novela Chanda Chema, tamthilia Kigoda na mwongozo wa riwaya Nguu za Jadi. Kwa sasa, anashughulikia mkusanyiko wa hadithi fupi; Dosari na Hadithi nyingine.